25th September 2013
B-pepe
Chapa
Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), imewashauri wafanyabiashara wa China kuingia ubia na Watanzania kwa faida ya nchi zote mbili.
Mwenyekiti wa TPSF, Dk. Reginald Mengi, alitoa rai hiyo katika hafla ya kutiliana saini ya makubaliano ya kushirikiana kati ya TPSF na Umoja wa Wafanyabiashara wa China nchini Tanzania (CBCT).
“Tunapenda kuona wakishirikiana na wafanyabiashara wa Tanzania hasa katika uwekezaji wa viwanda kwa lengo la kusaidia maendeleo ya nchi hii,” alisema Dk. Mengi mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Alisema kama wawekezaji wa China watakuja na kuwekeza bila kuwashirikisha Watanzania, uwekezaji huo utakuwa wa upande mmoja na Watanzania wataendelea kuwa maskini.
Alitoa changamoto kwa wawekezaji wa China kuwekeza kwenye viwanda vya kuyaongezea thamani mazao ya Tanzania ili bidhaa zake zipelekwe kwenye masoko ya China na nchi mbalimbali na kuuzwa kwa bei nzuri.
“Pia wafanyabiashara wa China wafuate sheria za nchi wanapoingiza bidhaa zao na kuzingatia ubora,” alisisitiza.
Alisema makubaliano yaliyofikiwa kati ya CBCT na TPSF yatazidi kuchochea uhusiano mwema ya kijamii, kisiasa na kibiashara kati ya nchi hizo mbili. Naye Balozi wa China nchini, Lu Youqing, alisema China na Tanzania zina historia ndefu za urafiki.
“Tuna ushirikiano mkubwa na sasa uhusiano wa kibiashara yamekuwa makubwa sana,” alisema.
Alisema kwa sasa kuna wafanyabiashara zaidi ya 500 wa Kichina hapa nchini.
Alisema mahusiano ya kibiashara kati ya TPSF na CBCT ni chachu na ni moja ya hatua katika kukuza uchumi wa Tanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye, alisema wafanyabiashara wa China kupitia CBCT, wamesaini makubaliano hayo katika jitihada za kuimarisha ushirikiano na biashara hapa nchini.
Rais wa CBCT, Zuang Zaisheng, alisema uhusiano huo wa kibiashara unalenga wafanyabiashara wa China na Tanzania kuwa kitu kimoja kibiashara.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni