RAIS wangu, wa kale walisema heri ukae kimya jamii ikudhanie kuwa wewe ni mpumbavu, kuliko useme, na ukaithibitishia jamii kuwa wewe ni mpumbavu.
Kwa ajili hiyo, leo nimeamua niseme kidogo, lakini kwa nguvu zaidi kuonyesha kusikitishwa na kauli iliyotishia kulichukulia hatua gazeti lililoandika kuwa ‘serikali yanuka damu’. Nasema huku ni kuweweseka. Yatafungiwa magazeti mangapi?
Kuweweseka ni matokeo ya fukuto ndani ya moyo linaloletwa na kumbukumbu ya uovu uliotendwa. Kamusi ya Kiswahili sanifu iliyochapishwa na Oxford toleo la pili inatafsiri neno weweseka kama kubabaika au kusema kama vile mtu asemavyo katika ndoto. Kusema serikali yako inaweweseka ni kusema serikali yako inababaika!
Kwa tafsiri hiyohiyo kubabaika ni kuwa na wasiwasi, kutokuwa na makini, kutaharuki, kuyugayuga au kupaparika. Kuwa na sifa hizi ni ishara ya upungufu mkubwa katika utendaji. Serikali kudhihirisha kuwa na hali kama hiyo ni kujitafutia muhali, kuleta kutoelewana au bughudha baina ya watu.
Rais wangu, juma lililopita gazeti moja lilikuwa na kichwa cha habari kilichoandikwa kwa herufi kubwa, ‘Serikali yanuka damu’. Kichwa hicho cha habari kilipambwa na picha za watu wanne.
Ni karibu sawa na miujiza kuwa siku ya tukio wanawema hawa hawakufa! Najua siku moja watakufa kwa sababu imeandikwa kuwa kila nafsi itauonja umauti!
Wenye kuamini katika uwepo wa Mwenyezi Mungu watakwambia kuwa hawa hawakufa siku hiyo kwa sababu siku yao waliyopangiwa na Muumba wao kufa, ilikuwa haijatimia! Lakini wako pia watakaokwambia kuwa huenda wakaja kufa kabla ya siku waliyopangiwa na Muumba wao kufika kutokana na ubovu ambao miili yao imetiwa na watesi wao!
Rais wangu, nawaombea afya njema wanawema hawa. Siku yao ya kuutoka ulimwengu huu wa mateso siijui kama ambavyo hata siku yangu mwenyewe pia siijui. Basi wacha niwalilie sasa na pia nijililie na mimi mwenyewe! Waliowatendea unyama huu mimi siwahukumu kwa sababu kuhukumu ni kazi yake Mungu. Watende lakini wajue kuwa hukumu ya Mwenyezi Mungu imesimama juu ya vichwa vyao.
Wajue pia kuwa hawataishi milele kusema watabaki kuilinda dunia, siku yao pia itafika nao watasimama mbele yake yeye aliye Muumba wao wote, wao watesi na wateswa wao. Siku hiyo, itakuwa ngumu kwao. Itakuwa siku ya kihoro. Mungu ni wa ajabu. Amewapangia kila mtu siku yake na atasimama mbele ya haki akiwa peke yake!
Nafsi zao zitawasuta na kuwajaza mateso ya uchungu mioyoni mwao yatokanayo na kuyakumbuka mateso waliowafanyia waja wa Mwenyezi Mungu. Nyongo itawakata maini watakapowaona wateswa wao wakiwa upande wa pili wa baba yao wakiimba na kumtukuza Mungu! Watatamani wawaombe msamaha kwa unyama waliowafanyia, lakini watakuwa wamechelewa!
Rais wangu, kwa sababu wahanga hawakuwanyang’anya mali yoyote waliokuwa nayo siku waliowafanyia unyama huo, basi lengo la uovu huu halikuwa ujambazi. Ndiyo kusema waliotenda unyama huu, hawakuwa majambazi. Sababu hii ndiyo inaitaka serikali iwajibike zaidi ili kujitoa katika tuhuma hizi zinazoelekezwa kwake.
Hata kama serikali itasema haikutenda unyama huu, kule kutowakamata wahusika kunawasukuma wananchi kuiona serikali yao kuwa mshirika katika kuwatesa na hata kuwaangamiza! Kwa ulinzi na upelelezi dhaifu kama huu, ni mwananchi gani atajiona yuko salama?
Ndugu rais, picha zilizowekwa gazetini zilikumbusha machungu mengi. Ilianza ya Absalom Kibanda. Alikuwa hana jicho moja. Lingine liling’olewa kinyama! Namfahamu Absalom. Alihariri makala zetu pale Free Media. Alifuatiwa na Steven Ulimboka akiwa mahututi! Amevimba mwili mzima! Kwa mara ya kwanza nimemwona Ulimboka uso kwa uso mwezi uliopita.
Nina kawaida ninaporudi kijijini kwangu Mbagala huwa napitia kijiwe changu cha zamani pale Uwanja wa Taifa. Kumbe siku hiyo Yanga walikuwa wanacheza. Sikuona mahali pa kuegesha mkweche wangu. Nikajikuta naitwa Mwalimu Mkuu njoo uweke hapa. Palikuwa na magari mengine. Nikamuuliza yule mtu, nikiegesha hapo hao nitakaowaziba watatokaje? Akaniambia weka tu najua wewe huendi mpirani. Sijui alijuaje. Mara ya mwisho nilienda Uwanja wa Taifa kuangalia mpira mwaka 1976.
Kwa mbele yangu kulikuwa na mwingine naye akiegesha gari lake. Aliposhuka nikamfananisha kisha nikamuuliza kama ndiye Steven Ulimboka, akasema ndiye. Nikamwomba nimsalimilie akanikubalia halafu hao wakaenda zao.
Sheikh Soraga na Padri Mwang’amba miili yao ilikuwa imeharibiwa vibaya. Unyama uliojidhihirisha wazi. Hawa nimewafahamu kupitia vyombo vya habari baada ya kukumbwa na majanga.
Rais wangu, ulimwengu umeendelea kujiuliza wana hawa walikosa nini hata kuwafanya wastahili adhabu ya mateso makali hivi? Walimkosea nani mkatili kiasi hiki? Hadi leo haijajulikana! Na kama aliyekosewa ndiye aliyetoa adhabu hizi, pia, hadi leo haijajulikana! Serikali imesema haihusiki. Aliyesema serikali inahusika ni nani? Huku ni kuyugayuga au kupaparika kunakosababisha kubabaika na hivyo kuifanya serikali ionekane inaweweseka.
Wa kuchonga hawakosekani hata msibani! Siku iliyofuata akatokea wa kutokea akasema kichwa kile cha habari kimeihusisha serikali na unyama ule. Akaahidi kuwa gazeti hilo litashughulikiwa kwa maana ya kulishikisha adabu! Haikujulikana mara moja kama mtu yule alikuwa anasema kwa kutumwa na serikali au alikuwa anajisemea mwenyewe. Kama alitumwa na serikali kwa hakika hiyo ni bahati mbaya. Anawafanya wanaosema serikali inaweweseka waonekane wanasema kweli. Kama alikuwa anatoa tu yake ya moyoni, basi ashindwe na alegee!
Rais wangu, wanasema kila mamlaka hutoka kwa Mungu. Ina maana kwamba Mwenyezi Mungu ameikabidhi serikali yetu wajibu wa kutunza na kulinda usalama na uhai wa watu wake walioko ndani ya nchi hii. Yanapotokea maafa kama haya yaliyowapata waja wake, Mwenyezi Mungu lazima amkamate au amuulize yule aliyemkabidhi dhamana ambaye ni serikali. Kama Mungu mwenyewe ataituhumu serikali kwa hili, wewe ni nani utake kuitoa serikali katika tuhuma hizi?
Sehemu zote tumeona, unapotokea uhalifu au wizi wa fedha au mali kwenye makampuni, viwanda au kwenye mashirika wa kwanza kukamatwa ni yule aliyekabidhiwa dhamana ya kutunza fedha au mali hiyo. Atashikiliwa hadi wahalifu wapatikane. Katika hali kama hii jitihada zozote zinazofanywa ili kuiondoa serikali katika tuhuma hizi ni sawa na kuweweseka. Mwenye jukumu na nyenzo zote za kuwakamata wahalifu wa unyama huu ni serikali yenyewe. Itaendelea kutuhumiwa hadi itakapowakamata watuhumiwa. Inaposhindwa kuwakamata watuhumiwa wakati kila siku inawakamata watuhumiwa wa maovu mengine wananchi wamtuhumu nani? Lazima wataendelea kuituhumu serikali. Kudhani kuwa leo hii bado wananchi wanaweza kuendelea kubabaishwa na mawazo mafupi ni kuweweseka pia! Kwa sababu ni kazi ya serikali kuwakamata wahalifu wa unyama huu, serikali haiwezi kukwepa kutuhumiwa. Siyo sawa hata kidogo kuwatisha wanaoituhumu serikali. Itaendelea kutuhumiwa kwa matukio haya hadi hapo itakapowakamata wahalifu. Kumbe atuhumiwe nani!
|
|
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni