Polisi ya Kimataifa yaanza msako Kenya
Polisi ya kimataifa Interpol, imeanza msako leo dhidi ya mwanamke wa Kiingereza aliyepewa jina la “ Mjane mweupe” baada ya kutolewa waranti wa kukamatwa kufuatia shambulizi la kigaidi katika jengo la kibiashara la Westgate katika mji mkuu wa Kenya Nairobi. Samantha Lewthwaite aliyesilimu na mwenye umri wa miaka 29 aliolewa na Germaine Lindsay mmoja wa washambuliaji wanne Wakiislamu waliojiripua kwa mabomu walipoushambulia mtandao wa usafiri wa chini ya ardhi mjini London Julai 7 mwaka 2005 na kuwauwa watu 52.Polisi ya kimataifa imesema mwanamke huyo, mama wa watoto watatu, anatakiwa na Kenya kujibu mashitaka ya kumiliki miripuko na kula njama ya kufanya hujuma tangu Desemba 2001. Awali Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Kenya Amina Mohammed alisema mwanamke mmoja wa Kiingereza alikuwa mmoja wa washambuliaji, ingawa Rais Uhuru Kenyatta alisema baadae kwamvba ripoti hizo hazikuthibitishwa. Wizara ya kigeni ya Uingereza na polisi ya nchi hiyo imekataa kusema lolote, ikisisitiza kwamba hilo ni suala la polisi ya kimataifa na maafisa wa Kenya.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni