TANGAZO

TANGAZO
WEKA TANGAZO LAKO HAPA

Jumapili, 29 Septemba 2013

Mashambulizi ya ash- Shabab katika kambi ya wakimbizi ya Daadab Kenya






wwwbinhafidhi.blogspot.comWimbi la mashambulio ya kundi la ash- Shabab la Somalia katika nchi jirani lingali linaendelea. Katika hatua yao ya hivi karibuni wanamgambo wa ash- Shabab wameshambulia kambi ya wakimbizi ya Daadab huko kaskazini mwa Kenya. Ripoti zinaeleza kuwa watu watatu wameuliwa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mashambulizi hayo. Imeelezwa kuwa wafanyakazi wa shirika moja la kimataifa la huduma za kibinadamu pia wamelengwa kwa mashambulizi hayo ya ash-Shabab.
Kambi ya wakimbizi ya Daadab iko katika mpaka wa Kenya na Somalia na ndio kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani. Maafisa usalama wa kieneo wameeleza kuwa wavamizi wa ash-Shabab walikuwa wamejizatiti kwa silaha za aina mbalimbali na mada za milipuko na waliingia kwa nguvu kambini hapo. Kambi hiyo inawahifadhi wakimbizi wengi wa Kisomali wasio na ulinzi waliokimbia ukame na mapigano ya ndani nchini kwao.
Jumamosi iliyopita pia watu wengi waliuliwa na wengine kujeruhiwa katika mashambulizi yaliyofanywa na kundi hilo hilo la ash-Shabab katika jengo la maduka la Westgate jijini Nairobi, Kenya.
Tangu mwaka jana wanamgambo wa kundi la ash-Shabab walianza kupoteza ngome zao muhimu nchini Somalia na kulazimika kurudi nyuma baada ya kupata kipigo kutoka kwa vikosi vya majeshi ya Umoja wa Afrika vilivyopelekwa nchini humo kusaidia serikali ya Mogadishu. 
Wakati huohuo kufukuzwa wanamgambo wa ash-Shabab katika bandari ya kistratijia ya Kismayu ambayo ilikuwa moja ya ngome zao kuu, kulikuwa na umuhimu mkubwa. Hii ni kwa sababu sehemu kubwa ya mahitaji ya silaha na chakula ya wanamgambo wa ash-Shabab ilikuwa ikidhaminiwa kupitia bandari hiyo.
Harakati za kundi hilo la ash Shabab zimezilazimisha nchi mbalimbali za Kiafrika kuchukua tahadhari kubwa za kiusalama. Huko Uganda vikosi vya usalama vimejiweka tayari kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi yoyote yanayoweza kufanywa na kundi hilo. Miongoni mwa hatua hizo ni kufungwa kamera kwenye maeneo ya umma, barabarani na katika baadhi ya majengo na vilevile kuimarishwa hatua za kiulinzi kwenye mipaka ya Uganda.
Uganda ni miongoni mwa nchi zilizochangia wanajeshi katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika huko Somalia. Kundi la ash-Shabab linapinga vikali uingiliaji wa vikosi vya majeshi ya kigeni huko Somalia na linataka vikosi hivyo viondoke katika ardhi ya nchi hiyo. Awali wanamgambo wa ash-Shabab walitishia kwamba watalipiza kisasi iwapo vikosi vya nchi za kigeni havitaondoka Somalia.
Mlipuko wa bomu uliotokea Kampala mji mkuu wa Uganda wakati watu walipokuwa wakitazama fainali za mpira wa miguu za Kombe la Dunia mwaka 2010 zilizofanyika Afrika Kusini na kuua  watu 76, ni mfano mmoja wa hatua za kulipiza kisasi za kundi la kigaidi la ash-Shabab huko Uganda. Wanamgambo wa ash-Shabab wamedai kuwa, wanajeshi wa Kenya wameondoka huko Somalia kutokana na hali mbaya ya usalama inayoikabili Kenya, madai ambayo yamekadhibishwa na viongozi wa Nairobi.  
Swali linaloulizwa kwa sasa ni kuwa, ni nani anayewafadhili na kuwadhaminia wanamgambo wa ash-Shabab silaha na mahitaji mengine muhimu?  Wakati huo huo weledi wa mambo wanasema kuwa ukosefu wa amani katika eneo la Pembe ya Afrika unayafaidisha madola ya Magharibi ambayo yatatumia fursa hiyo kwa ajili ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi za eneo hilo.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni