Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa viongozi wa Marekani wanapaswa kuamiliana na Iran kwa kutilia maanani uhakika wa mambo na kuliheshimu taifa la nchi hii
.
Marziye Afkham ameyasema hayo katika mazungumzo yake na waandishi habari wa ndani na nje ya nchi akijibu matamshi yaliyotolewa na Rais Barack Obama wa Marekani baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel Benjamin Netanyahu. Obama alisema kuwa chaguo la mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran bado liko mezani.
Msemaji wa Wizara ya mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa hii leo serikali ya Marekani inakabiliwa na mtihani mkubwa kwamba ni kwa kiwango gani inaweza kusimama kidete mbele ya mashinikizo ya wapenda vita; kadiri uwezo huo utakavyokuwa mkubwa ndivyo itawezekana kuchunguza uwezekano wa kuamiliana na Marekani.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema hatupasi kusahau kwamba mashinikizo ya utawala haramu wa Israel ni kutokana na kutengwa utawala huo na hasira yake dhidi ya mafanikio ya siasa za serikali ya Tehran katika uwanja wa kimataifa.
Kuhusu mwenendo wa mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran amesema mazungumzo yajayo kati ya pande hizo mbili yataainisha fremu ya mwenendo huo na harakati za baadaye. Marziye Afkhami amesema miongoni mwa matakwa ya Iran ni kutambuliwa rasmi shughuli za nyuklia na kufutwa vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Iran.
Kuhusu madai ya kukamatwa jasusi Muirani Mbelgiji huko Israel, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema madai kama hayo yamekuwa wakitolewa mara kwa mara na kwamba kutolewa kwake mara hii sambamba na safari ya Benjamini Netanyahu huko Marekani kuna lengo la kuiondoa Israel katika hali ya kutengwa kimataifa.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni