Tume ya Mabadiliko ya Katiba imelishangaa Bunge kwa ‘undumila kuwili’ wake wa kupitisha sheria mbili zinazokinzana kuhusiana na mchakato unaosimamiwa na tume hiyo.
Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari, kwa lengo la kuwapa taarifa ya uendeshaji wa Mabaraza ya Katiba, ngazi ya serikali za mitaa ulivyofanyika.
Warioba alisema mikutano hiyo iliyoendeshwa na Tume ilianza Julai 12, 2013 na kumalizika Septemba 2, mwaka huu.
Alisema wakati Sheria Mama iliyoiunda Tume ya yake mwaka 2011 inatamka kwamba Tume iendelee kuwapo katika mchakato wote, hadi pale kura ya maoni ya kupitisha au kukataa Katiba mpya itakapofanyika.
Hata hivyo, alisema Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013 uliopitishwa katika mkutano wa Bunge wa 12, umekataa hilo.
Muswada huo uliungwa mkono na kupitishwa na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM ) na Augustine Mrema (TLP), lakini wabunge wa upinzani wa Chadema,CUF na NCCR-Mageuzi waliupinga na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge.
Jaji Wariona alisema marekebisho yaliyofanywa katika kikao cha 12 yanakinzana na Sheria mama kwa sababu, Muswada wa sasa unataja muda wa Tume kumalizika pale itakapowasilisha Rasimu ya Katiba, katika Bunge Maalum la Katiba.
“Tunajua kazi ya kutunga sheria si ya kwetu, ni ya wengine, na hata sheria inayotuongoza katika utendaji kazi wetu, tumeikuta ikiwa imeshatungwa tayari na wahusika, na hakika sisi tunafanya kazi kulingana na sheria iliyo mbele yetu,” alisema.
Jaji Warioba alisema hata hivyo kwamba, wakati Muswada wa Marekebisho unahitimisha ukomo wa Tume baada ya kuwasilisha Rasimu katika Bunge Maalumu la Katiba, Sheria mama inawataka waendelee mpaka kwenye hatua ya kura ya maoni.
Alisema Sheria mama inaitaka Tume iendelee mpaka kwenye hatua hiyo, ili pamoja na mambo mengine iweze kutoa elimu kwa wananchi.
“Sasa utafanya jukumu hilo kwa kutumia mamlaka ipi, wakati tayari shughuli zako zimefikia ukomo baada ya kuwasilisha Rasimu kwenye Bunge Maalum la Katiba?” alihoji Jaji Warioba.
KUJIUZULU WAJUMBE WA TUMEJaji Warioba alizungumzia pia taarifa zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari za baadhi ya wajumbe wa Tume kutishia kujiuzulu kama ishara ya kupinga Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliopitishwa na Bunge hivi karibuni.
“Siyo kweli kuwa wanataka kujiuzulu. Kilichotokea ni kuwa baada ya safari ya kuzunguka karibu nchi nzima, na kukutana na changamoto nyingi ambazo ziliwachosha, zikiwemo za matamshi ya Kuwadhalilisha,” alisema.
Alisema baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa walitoa matamshi yaliyolenga kuwadhalilisha wajumbe wa Tume, na kuishusha thamani kazi iliyofanywa na Tume ya kuandika Rasimu ya Katiba.
“Aidha baadhi ya viongozi wa siasa pia walitoa matamshi yaliyowalenga wajumbe wa Tume, na kuwafanya baadhi ya wajumbe wa Mabaraza, kuwajadili wajumbe wa Tume, badala ya Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume,” alisema.
Hata hivyo, Jaji Warioba hakutoa maelezo zaidi kuhusiana na matamshi yaliyotolewa dhidi ya wajumbe wa Tume yake.
Alisema ni katika vikao vya kupitia safari hizo za wajumbe na changamoto walizokumbana nazo pamoja na uchovu waliokuwa nao kutokana na changamoto hizo, ndipo baadhi ya wajumbe walipoonekana kusema bwana basi, lakini hawakusema wanataka kujiuzulu.
Alisema Katiba inayotafutwa ni ile itakayoleta umoja wa Watanzania wote na ambayo itakuwa chachu ya maendeleo ya nchi kwa vizazi vijavyo.
“Hatutafuti katiba ya kundi moja au ya chama kimoja, au katiba itakayotokana na mapambano, kwa hiyo ni muhimu kwa viongozi wa kisiasa, wakaona busara ya kukaa pamoja na kuondoa tofauti zao,” alisema.
Jaji Warioba alisema, katiba yenye kuleta umoja haitapatikana kwa njia ya maandamano au malumbano ya kwenye majukwaa, na badala yake itapatikana kwa njia ya kuzimaliza tofauti walizonazo, kwa njia ya mazungumzo.
IDADI YA MIKUTANOIli kuendesha mikutano ya Mabaraza ya Katiba kwa ufanisi, Jaji Warioba alisema Tume ilijigawa katika makundi 14, kila kundi likiwa na wajumbe wawili au watatu.
Alisema makundi hayo yalizunguka nchi nzima na kufanya mikutano 179, iliyohudhuriwa na wajumbe 19,337, ambayo ilifanyika katika kila Halmashauri ya wilaya, Halmashauri ya Manispaa na jiji, huku mkutano mmoja ukidumu kwa wastani ya siku tatu.
Alisema jumla ya mikutano 166 ilifanyika Tanzania Bara na 13 ilifanyika Tanzania Zanzibar.
CHANGAMOTOAlisema baadhi ya changamoto zilizojitokeza ni za baadhi ya vyama vya siasa kuingilia uhuru wa wajumbe katika kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya katiba.
Aidha, alizitaja zingine kuwa, ni kwenye baadhi ya maeneo, wajumbe wa Mabaraza ya Katiba walifundishwa nini cha kusema juu ya Rasimu ya Katiba, na baadhi ya vyama vya siasa kuendesha mikutano ya hadhara na ya ndani ya wanachama wao, sambamba na mikutano ya mabaraza.
KINACHOENDELEAJaji warioba alisema, kinachofanyika kwa sasa ni uchambuzi wa maoni yaliyotolewa na Mabaraza ya Katiba, kwa kufuata mwongozo ambao Tume imejiwekea na uchambuzi unafanywa kwa kuzingatia uzito wa hoja, zilizotolewa na wananchi katika maeneo tofauti ya Rasimu ya Katiba.
Alisema baada ya uchambuzi, Tume itaandaa Ripoti itakayojumuisha Rasimu ya Katiba iliyoboreshwa kutokana na maoni ya Mabaraza ya Katiba na kuiwasilisha kwa Rais wa Tanzania na wa Zanzibar, kama Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inavyolelekeza.
“Mipango ya Tume ni kukamilisha kazi hii ndani ya muda uliowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83,” alisema.
MJUMBE AITUMUMU CCMWakati Jaji Warioba akisema hayo, Mjumbe wa Tume hiyo, Dk. Sengondo Mvungi, amesema Chama Cha Mapinduzi) kinaandaa rasimu yake ya Katiba Mpya, ili kiiwasilishe kinyemela kupitia kwa wabunge wake kwenye Bunge la Katiba litakalofanyika Novemba mwaka huu.
Alisema kuwa rasimu hiyo ni tofauti na iliyotolewa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwamba kutokana na hali hiyo, yuko tayari kujiuzulu ujumbe katika tume hiyo ili kuepukana na aibu kutokana na CCM na serikali kuamua kuvuruga kwa makusudi mchakato wa kupata katiba mpya inayokidhi matakwa ya wananchi wote.
Aliliambia NIPASHE jana kuwa ni aibu kubwa kwa CCM kuamua kuandaa rasmu yake huku kikijua chombo kilichopewa mamlaka hayo ni Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kushiriki maadhimisho ya miaka 18 ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na kusema kuwa anazo taarifa za uhakika kwamba mpango huo wa CCM umeandaliwa na makada wa chama na umeishakamilika hivi sasa.
Dk. Mvungi alisema CCM kimemaliza kuandaa rasimu hiyo na kwamba kitaiwasilisha katika Bunge la Katiba na wabunge wake wamejipanga kuitetea mpaka ipite.
Alisema hali ni mbaya kwa tume kwa kuwa imeingiliwa na CCM na serikali yake na kwamba mambo yakiendelea hivyo, wake watajiondoa.
Amesema kwa upande wake yupo tayari kujiuzulu na kukaa pembeni badala ya kuendelea kupata aibu huku Watanzania wakimtazama.
“Mimi nipo tayari, nasubiri wajumbe wenzangu, wakisema kujiondoe hata sasa mimi nipo tayari kufanya hivyo kwa kuwa sikuingia kule kutafuta fedha, bali kuwawakilisha wananchi,” alisema Dk. Mvungi
“Aina ya sasa iliyotumika kuandika Katiba hii imewachanganya CCM na serikali na sasa wameamua kuvuruga mchakato kwa makusudi,” aliongeza Dk. Mvungi.
Alitaja mambo matatu ambayo yanaichangana CCM na serikali ni pamoja na rasimu hiyo kutamka suala la kuwapo serikali tatu, mbunge kuwekewa ukomo wa vipindi vitatu vya miaka 15 na wabunge kutokuwa mawaziri.
KAULI YA MANGULAAkizungumzia tuhuma hizo, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula, alikanusha na kusema siyo za kweli.
Mangula baada ya kupokea simu jana jioni alisema alikuwa kwenye kikao Bagamoyo mkoani Pwani.
MAALIM SEIF: JK USISAINIMakamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hmad, amemuomba Rais Jakaya Kikwete kutousaini muswada huo badala yake ufanyiwe kwanza marekebisho.
Maalim Seif alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na Wazanzibari wanaoishi Tanzania Bara na kufafanua kuwa Wazanzibar hawakushirikishwa katika kutoa maoni.
Aidha, alisema Rasimu ya Katiba mpya inapaswa kutamka Serikali ya Tanganyika badala ya Tanzania Bara katika mfumo wa Muungano wa serikali tatu za Zanzibar, Tanganyika na Shirikisho.
Imeandikwa na Raphael Kibiriti, Richard Makore na Muhibu Said.