Harakati za kuuhamasisha umma kupinga mchakato wa mabadiliko ya katiba kuhodhiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimepamba moto, baada ya Waziri wa Katiba na Sheria wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Abubakari Khamisi Bakari, kuwataka Wazanzibari kutouunga mkono kwa madai kwamba, hawakushirikishwa.
Amesema iwapo serikali italazimisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba kuendelea bila kuwashirikisha Wazanzibari katika kuutolea maoni Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2013, hawatakubali kwenda kwenye Bunge Maalum la Katiba.
Alisema hayo alipokuwa akihutubia maelfu ya watu katika mkutano wa hadhara, ambao ni mwendelezo wa harakati hizo, uliofanyika katika Uwanja wa Demokrasia Kibandamaiti, mjini hapa jana.
Harakati hizo zilizinduliwa na vyama vya CUF, Chadema, NCCR Mageuzi, katika viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam, Jumamosi wiki iliyopita.
Alisema Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai; Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, wamewahadaa Wazanzibari na kuudanganya umma kwamba, Wazanzibari walishirikishwa katika kuutolea maoni muswada huo wakati si kweli.
Aliwataka wabunge kutumia kanuni za Bunge kumchukulia hatua Ndugai kwa kulidanganya Bunge, vinginevyo awajibike kwa kujiuzulu.
Alisema pia kitendo cha Waziri Chikawe kueleza kwamba, Wazanzibari walishirikishwa katika kuutolea maoni Muswada huo, kimeonyesha kuwa ni mwongo.
Bakari alisema Wazanzibari hawakushirikishwa katika hilo, badala yake kilichofanywa na serikali pamoja na Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria ni kuilaghai Zanzibar.
Alisema awali, Wazanzibari walipelekewa marekebisho ya muswada huo yakiwa na vifungu vinne pekee wakitakiwa wavitolee maoni.
Kwa mujibu wa Waziri Bakari, yeye binafsi alivipitia vifungu hivyo na kushauriana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kabla ya kuvitolea maoni.
Alisema baada ya kuvipitia vifungu hivyo, alimwandikia barua Makamu wa Pili wa Rais wa SMZ, Balozi Seif Ali Iddi, na kumueleza kwamba, hawana matatizo na vifungu hivyo.
Alisema baada ya kumueleza hivyo Makamu huyo wa Rais, naye (Makamu wa Rais) alimwandikia Waziri Mkuu barua kumueleza maoni hayo ya Wazanzibari kuhusu vifungu hivyo.
Alisema hata hivyo, kitendo hicho cha Makamu wa Pili wa Rais wa SMZ, kilikuwa ni hadaa, kwani baadaye, walikwenda wakarekebisha vifungu 12 na kuvipeleka bungeni bila kuwashirikisha Wazanzibari kuvitolea maoni.
Alisema kitendo cha Ndugai kuwaonyesha wabunge bungeni barua hiyo ya Makamu wa Pili wa Rais wa SMZ na kusema kuwa Wazanzibari walishirikishwa kimeonyesha kuwa ni mwongo.
Alisema Wazanzibari walishirikishwa katika kuvitolea maoni vifungu vinne tu vya Muswada huo, lakini hawakushirikishwa kabisa katika kuvitolea maoni vifungu 12.
Alisema baadaye Chikawe na Lukuvi, walikweda Zanzibar kumuona (Waziri Bakari) wakitaka wajadili vitu vingine bila kuwapa muswada, hivyo akalikataa hilo kwa maelezo kwamba, hayuko tayari kuiuza Zanzibar.
“Halafu wanatoka hapa wanakwenda kudanganya bungeni kwamba, waliwashirikisha Wazanzibari, waongo hawakutushirikisha,” alisema Waziri Bakari.
Alisema wanaupinga Muswada huo kwa kuwa kuna vifungu vinawaumiza Wazanzibari, ikiwamo kiwango cha wapigakura Wazanzibari kuipitisha Rasimu ya Katiba.
“Hivyo, itapita katiba ile ile wanayoitaka CCM. hayo hatuyakubali hata kidogo. Hatukushirikishwa, katiba hii itawaumiza. Na yeyote Mzanzibari atakayeikubali hana akili,” alisema.
Aliwataka Wazanzibari kutoikubali rasimu hiyo na kusema kama serikali italazimisha basi hawatakubali kwenda kwenye Bunge la Katiba.
Mbunge wa Mkoani (CUF), Ali Khamis, alisema serikali haiko wazi katika kuendesha mchakato huo, hivyo akawataka wananchi kuwaunga mkono kuupinga. Mkurugenzi wa Katiba na Sheria wa Chadema, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alisema bila katiba mpya hakuna Zanzibar huru na pia bila Zanzibar mpya hakuna katiba huru.
Alisema tangu mwaka 1964, Zanzibar imenyangánywa sauti yake katika Muungano.
Lissu alisema wananchi wa Tanganyika na Zanzibar hawakuulizwa kwa njia yoyote nchi hizo kuungana.
Lakini alisema baada ya miaka hiyo, leo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linataka kutunga katiba bila kuwashirikisha Wazanzibari.
Alisema pia kwa miaka yote mambo ya Muungano yameongezwa bila kuwashirikisha Wazanzibari, lakini wakipewa vyeo, au kuwekwa vizuizini wananyamaza.
Lissu alisema ilipofika miaka ya 1984, walipoona Wazanzibari wanakuja juu, walianza kutumia mabavu kuwanyamazisha.
“Hivyo, kilichotokea Dodoma siyo kitu kigeni, ni mwendelezo wa mambo ya miaka 1960," alisema Lissu na kuongeza kuwa mambo hayo hayatakoma bila kuiondoa CCM madarakani.
Lissu alisema Dodoma wamechakachua sana na kusema iwapo Wazanzibari watanyamaza basi watakumbana na masaibu mbalimbali, ikiwamo kupunjwa idadi ya wajumbe watakaounda Bunge Maalum la Katiba na hivyo, kushindwa kujinusuru na unyongaji unaofanywa na serikali ya CCM dhidi yao.
Alisema pia iwapo wataruhusu na kufika hadi kwenye hatua upigaji kura ya maoni, basi watachakachuliwa kupitia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohammed Habib Mnyaa, alisema kinachotaka kufanywa na CCM ni kutaka kuvuruga mchakato wa serikali tatu.
ALICHOSEMA MBATIA
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema tunu za Watanzania ni pamoja na utu, uzalendo, uwazi na lugha ya taifa, hivyo aliwataka kuhakikisha inapatikana katiba itakayoridhiwa na wote.
Alimuomba Rais Jakaya Kikwete kuzingatia ushauri uliotolewa na Waziri Bakari kwa kutosaini Muswada huo na kurudishwa bungeni ili ufanyiwe marekebisho ili kuliunganisha taifa.
MBOWE ANENA
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema wamegundua Muungao ni mradi, ambao unatumiwa na kikundi cha watu wachache walioko Tanzania Bara na wengine Zanzibar.
Hivyo, akawataka Wazanzibari kuungana na wenzao wa Dar es Salaam, ambao alisema wamekubali kushiriki ama katika maandamano au mgomo unaoweza kuitishwa nchini kote Oktoba 10, mwaka huu, kudai katiba inayotakiwa na wananchi wote.
KAULI YA LIPUMBAMwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema anamsikitikia Balozi Iddi kwa kukubali kushiriki katika kulidanganya Bunge kwamba, Wazanzibari walishirikishwa katika kuutolea maoni muswada huo, akisema kitendo hicho ni sawa na yeye alichakachuliwa bungeni.
Alisema kinachofanywa na wasaidizi wa Rais Kikwete ni kumtakia mabaya, kwa kuwa iwapo atausaini muswada huo na kuwa sharia, mchakato wa katiba utakuwa umekwisha.
“Hivyo, tusikubali watu wachache wakatuzuia kupata katiba inayoridhiwa na inayotokana na wananchi wenyewe,” alisema Profesa Lipumba.
HOJA ZA WAPINZANIKwa mujibu wa Lissu, wanachopinga katika muswada huo ni mapendekezo ya kumpa Rais mamlaka ya kuteua wajumbe 166 wa Bunge Maalum la Katiba kwani mapendekezo haya yanarudisha dhana kwamba wajumbe hao watakuwa watu wa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM.
“Rais Kikwete na chama anachokiongoza ni wadau wakubwa wa mchakato wa Katiba Mpya na wana maslahi halisi na makubwa ya kuhakikisha kwamba matakwa ya chama chao ndio yanakuwa Katiba Mpya ya nchi yetu, sasa anapopewa mamlaka ya kuteua wajumbe wa Bunge la Katiba inakuwa siyo sahihi ni wazi kuwa katiba mpya itakuwa ya Ki-CCM…CCM,” anasema.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, anasema hoja ya pili ambayo wanaipinga ni shinikizo kutoka kwa wabunge wa CCM ambao wanataka Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuvunjwa, jambo ambalo wanaliona halina nia njema kwani wanaamini linatokana na chama tawala kutofurahishwa na Rasimu ya kwanza ya katiba iliyoandaliwa na tume hiyo.
Alisema wanashtushwa na uamuzi huo kwa sababu wabunge walipitisha bajeti ya Sh. bilioni 34 kwa ajili ya kuiwezesha tume hiyo kukamilisha mchakato wote wa katiba sasa wabunge wa CCM wanapopitisha sheria ya kuitaka tume ivunjwe siyo jambo zuri.
Hoja ya tatu ni kuhusu uwakilishi katika Bunge Maalum la Katiba, ambayo kwa mujibu wa Lissu, hakuna uwiano kati ya Tanzania Bara na Visiwani wakati Zanzibar nayo ni nchi, hivyo wananchi walitegemea kuwa na idadi sawa ya wajumbe katika bunge hilo.
“Wabunge wanaotoka Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano ni 83 wakati Baraza la Wawakilishi Zanzibar lina wajumbe 76. Kwa hiyo, ili kutekeleza matakwa ya kifungu cha 22(1) na (2) cha Sheria, Zanzibar itakuwa na wajumbe 219 katika Bunge Maalum lenye wajumbe 604, sawa na takriban asilimia 36 ya wajumbe wote wakati Tanzania bara watakuwa ni asilimia 64,” anasema.Anasema kwa kuwa inatengenezwa katiba ya nchi mbili, kunahitajika kuwa na uwiano sawa wa wajumbe kwenye Bunge la Katiba.