TANGAZO

TANGAZO
WEKA TANGAZO LAKO HAPA

Alhamisi, 26 Septemba 2013

AL SHABAAB WATISHIA KUIVAMIA TANZANIA








*Polisi nchini wasema vyombo vya ulinzi viko macho*Mtanzania akamatwa Kenya akihofiwa gaidiWAKATI wananchi wa Afrika Mashariki wakijawa na hofu ya mashambulio yanayopangwa kufanywa na vikundi vya ugaidi vya Al Qaeda na Al Shabab, imebainika kuna Watanzania waliopewa mafunzo ya ugaidi wanaojiandaa kufanya maovu.Hayo yamebainika siku chache baada ya wanamgambo wa kundi la Al Shabab kufanya mashambulio katika Jengo la Biashara la Westgate mjini Nairobi na kuua watu zaidi ya 70 na kuacha mamia wengine wakiwa wamejeruhiwa.Mkuu wa Interpol Tawi la Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav Babile aliyasema hayo jana katika mahojiano maalumu na MTANZANIA.Alikuwa akizungumzia kauli ya hivi karibuni iliyotolewa na Msemaji wa Al Shabab, Sheikh Abdulaziz Abu Muscab aliyetoa tahadhari kwamba kundi lake linapanga mashambulio mengine Tanzania na Uganda.Babile alisema taarifa zinaonyesha vijana wa Tanzania waliojiunga na mafunzo ya ugaidi yanayotolewa na vikundi vya Al Qaeda na Al Shabab, wamefanya hivyo baada ya kushawishiwa watapata utajiri wa haraka.Alisema hali hiyo imevifanya vyombo vya ulinzi na usalama nchini kutoipuuza kauli hiyo ya Sheikh Abdulaziz Abu Muscab.“Tunajua wapo Watanzania wanapewa dozi za ugaidi, na sisi siyo kisiwa, watu ni hao hao… tumejipanga kuyakabili haya na kuushirikisha umma katika ulinzi,” alisema.Babile alisema kauli ya msemaji wa kundi la Al Shabab ya kuivamia Tanzania siyo ya kupuuza na kusisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini viko tayari kukabiliana na lolote litakalotokea.“Tumeisikia kauli yake kwenye mitandao ya jamii, imetufanya kuwa alert (macho) vya kutosha, imetuweka sawa na imetukumbusha kuwa tunaweza kuvamiwa wakati wowote.“Hatuja-relax hata kidogo, tumejiweka sawa kwenye human resources zetu, materials resource na hata frontline officers wetu wako makini mno.“Mfano kwenye viwanja vya ndege ambako ni muhimu, kuna mitambo inayoweza kugundua hati za kusafiria za washukiwa wa uhalifu wanaotafutwa kimataifa na tutawakamata tu.“Lakini hata kwenye mipaka yetu yote hatuko peke yetu, tumepanua wigo wa kupata taarifa za kiintelijensia na katika kufanya kazi hii tunashirikiana na vyombo vyote vya ulinzi na usalama,” alisema.Baada ya kufanya mashambulio mjini Nairobi Jumamosi iliyopita, Msemaji wa Al Shabab, Sheikh Abdulaziz Abu Muscab, aliripotiwa kwenye mitandao ya jamii akisema shambulio hilo lilikuwa ni la kulipiza kisasi baada ya majeshi ya Kenya kuvamia kundi hilo lenye makazi yake mjini Kismayu, Somalia.Mitandao ya jamii pia ilimnukuu Sheikh Abu Muscab akijigamba kuwa wakati wowote mashambulio ya kikundi hicho yataelekezwa Uganda na Tanzania.Wakati huohuo, Babile amesema Mtanzania mmoja alikamatwa Kenya akishukiwa kuwa ni mmoja magaidi waliovamia jengo la Westgate. Bila kumtaja jina, alisema mtu huyo ni mkazi wa Arusha na alikamatwa muda mfupi baada ya kuingia Kenya akitoa Tanzania, akitumia usafiri wa mabasi ya abiria.“Walipomkamata wakatuletea taarifa sisi, tukatafuta kwenye database zetu na information za ndani zikatuonyesha hakuwa mtu hatari, tukamuachia.“Kilichowatia hofu na kumshuku mtu huyu ni muda alioingia Kenya na muda wa tukio lilipotokea… lakini tumeangalia taarifa zote tukagundua hakuwa na shaka,” alisema Babile.


Jumatano, 25 Septemba 2013

`Wafanyabiashara wa China shirikianeni na Watanzania`


25th September 2013
Chapa
Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa (kulia), akimkabidhi Mkurugenzi Mwendeshaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Godfrey Simbeye, kitabu cha Mwongozo wa Kampeni kwa Umma kuhusu Soko la Kukuza Ujasiriamali (EGM),jijini Dar es Salaam jana.


Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), imewashauri wafanyabiashara wa China kuingia ubia na Watanzania kwa faida ya nchi zote mbili.

Mwenyekiti wa TPSF, Dk. Reginald Mengi, alitoa rai hiyo katika hafla ya kutiliana saini ya makubaliano ya kushirikiana kati ya TPSF na Umoja wa Wafanyabiashara wa China nchini Tanzania (CBCT).

“Tunapenda kuona wakishirikiana na wafanyabiashara wa Tanzania hasa katika uwekezaji wa viwanda kwa lengo la kusaidia maendeleo ya nchi hii,” alisema Dk. Mengi mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Alisema kama wawekezaji wa China watakuja na kuwekeza bila kuwashirikisha Watanzania, uwekezaji huo utakuwa wa upande mmoja na Watanzania wataendelea kuwa maskini.

Alitoa changamoto kwa wawekezaji wa China kuwekeza kwenye viwanda vya kuyaongezea thamani mazao ya Tanzania ili bidhaa zake zipelekwe kwenye masoko ya China na nchi mbalimbali na kuuzwa kwa bei nzuri.

“Pia wafanyabiashara wa China wafuate sheria za nchi wanapoingiza bidhaa zao na kuzingatia ubora,” alisisitiza.

Alisema makubaliano yaliyofikiwa kati ya CBCT na TPSF yatazidi kuchochea uhusiano mwema ya kijamii, kisiasa na kibiashara kati ya nchi hizo mbili. Naye Balozi wa China nchini, Lu Youqing, alisema China na Tanzania zina historia ndefu za urafiki.

“Tuna ushirikiano mkubwa na sasa uhusiano wa kibiashara yamekuwa makubwa sana,” alisema.
Alisema kwa sasa kuna wafanyabiashara zaidi ya 500 wa Kichina hapa nchini.

Alisema mahusiano ya kibiashara kati ya TPSF na CBCT ni chachu na ni moja ya hatua katika kukuza uchumi wa Tanzania.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye, alisema wafanyabiashara wa China kupitia CBCT, wamesaini makubaliano hayo katika jitihada za kuimarisha ushirikiano na biashara hapa nchini.

Rais wa CBCT, Zuang Zaisheng, alisema uhusiano huo wa kibiashara unalenga wafanyabiashara wa China na Tanzania kuwa kitu kimoja kibiashara.

 

Wanawake wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kukutwa na maiti


Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova
Wanawake wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kukutwa na maiti iliyokuwa na dawa za kulevya tumboni.Watuhumiwa hao wametajwa na Jeshi hilo mkoani Dar es Salaam kuwa ni Nasra Omari (36) na Mwanaisha Kapama (36), ambao ni wakazi wa Kigogo Luhanga, jijini Dar es Salaam na kwamba walikutwa na maiti iliyokuwa na dawa za kulevya aina ya heroin pipi 33 zenye thamani ya mamilioni ya fedha.Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, alisema watu hao walikamatwa Septemba 21, mwaka huu katika eneo la Tabata.Kamishna Kova alisema alipata taarifa kuwa kuna mtu aliyefahamika kwa majina ya Rajabu Kidunda na Mashaka Mabruki  (43) ambaye ni mfanyabiashara aliyefika Dar es Salaam kutoka mkoani Mtwara kwamba alifariki dunia ghafla muda mfupi baada ya kutoka bafuni kuoga.Alisema makachero walifika eneo la tukio nyumbani kwa Nasra Omari Kigogo Luhanga na kuikuta maiti hiyo sebuleni ikiwa imelazwa chali katika godoro sakafuni.Alisema polisi waliupeleka mwili huo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa ajili ya uchunguzi.Kamishna Kova alisema uchunguzi huo ulifanywa na jopo la madaktari wawili na maofisa wa juu wa polisi pamoja na ndugu wa karibu wa marehemu.Alisema walipoipasua maiti walikuta pipi hizo zenye urefu wa sentimita sita. Hata hivyo, Kova alisema thamani yake ni ya mamilioni ya fedha na kwamba thamani halisi itatolewa na Mkemia Mkuu wa Serikali baada ya kukamilisha uchunguzi.Kwa mujibu wa Kamishna Kova, uchunguzi  unaonyesha kuwa marehemu alifika Dar es Salaam kutoka Mtwara Septemba 21 mwaka huu kwa maelezo kwamba alifika kwa ajili ya matibabu kwa kuwa alikuwa mgonjwa. Hata hivyo, mtu huyo alifariki siku hiyo hiyo aliyowasili jijini Dar es Salaam.“Inasemekana kwamba muda mfupi kabla ya kifo chake, marehemu alienda kuoga bafuni na aliporudi chumbani alifariki ghafla na ndipo polisi tulipata taarifa na kwenda kuchukua maiti na kuipeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili,” alisema Kova.Alisema, Pipi hizo zimehifadhiwa na kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ambaye atatoa ripoti na gharama za dawa hizo.Aidha, alisema kuwa marehemu alikutwa na hati ya dharura ya kusafiria ya nchi za nje ambayo haikuonyesha anakoelekea.Pia Kamanda Kova alisema marehemu alikutwa na vielelezo vingine kama fedha taslimu za Kenya Sh. 700 (T Sh. 13,300), Dola za Marekani 100 (162,000) na fedha za Visiwa vya Shelisheli 100.Kamishna Kova alisema kuwa watuhumiwa hao wanaendelea kushikiriwa na polisi kwa ajili ya mahojiano na kuwa baada ya kukamilika watafikishwa mahakamani.Wakati huo huo, Kamishna Kova aliwatahadharisha Watanzania kuwa makini na watu wanaowatilia shaka ili kuepusha uwezekano wa kutokea matukio ya ugaidi kama tukio la mashambulizi jijini Nairobi, Kenya Jumamosi iliyopita.“Watanzania tusiendelee kuwa wapole na tusimuamini mtu wa aina yeyote, kwa kuwa uaminifu siku hizi ni mdogo,” alisema na kuongeza:“Sisi na jeshi letu tutashirikiana na Idara ya Uhamiaji, taasisi nyingine pamoja na wadau mbalimbali kwa kuwafichua watu wasio na nia nzuri na nchi yetu,” alisema Kova.Aidha alisema kuwa wataweka ulinzi wa kutosha katika viwanja vya ndege, bandari na mahoteli makubwa.“Ukiona mwenzio ananyolewa na wewe tia maji, katika sehemu kama hotelini endapo mtu atatiliwa (ma)shaka wamiliki watoe taarifa kwa jeshi letu,” alisema. 

Serikali yako inaweweseka




RAIS wangu, wa kale walisema heri ukae kimya jamii ikudhanie kuwa wewe ni mpumbavu, kuliko useme, na ukaithibitishia jamii kuwa wewe ni mpumbavu.
Kwa ajili hiyo, leo nimeamua niseme kidogo, lakini kwa nguvu zaidi kuonyesha kusikitishwa na kauli iliyotishia kulichukulia hatua gazeti lililoandika kuwa ‘serikali yanuka damu’. Nasema huku ni kuweweseka. Yatafungiwa magazeti mangapi?
Kuweweseka ni matokeo ya fukuto ndani ya moyo linaloletwa na kumbukumbu ya uovu uliotendwa. Kamusi ya Kiswahili sanifu iliyochapishwa na Oxford toleo la pili inatafsiri neno weweseka kama kubabaika au kusema kama vile mtu asemavyo katika ndoto. Kusema serikali yako inaweweseka ni kusema serikali yako inababaika!
Kwa tafsiri hiyohiyo kubabaika ni kuwa na wasiwasi, kutokuwa na makini, kutaharuki, kuyugayuga au kupaparika. Kuwa na sifa hizi ni ishara ya upungufu mkubwa katika utendaji. Serikali kudhihirisha kuwa na hali kama hiyo ni kujitafutia muhali, kuleta kutoelewana au bughudha baina ya watu.
Rais wangu, juma lililopita gazeti moja lilikuwa na kichwa cha habari kilichoandikwa kwa herufi kubwa, ‘Serikali yanuka damu’. Kichwa hicho cha habari kilipambwa na picha za watu wanne.
Ni karibu sawa na miujiza kuwa siku ya tukio wanawema hawa hawakufa! Najua siku moja watakufa kwa sababu imeandikwa kuwa kila nafsi itauonja umauti!
Wenye kuamini katika uwepo wa Mwenyezi Mungu watakwambia kuwa hawa hawakufa siku hiyo kwa sababu siku yao waliyopangiwa na Muumba wao kufa, ilikuwa haijatimia! Lakini wako pia watakaokwambia kuwa huenda wakaja kufa kabla ya siku waliyopangiwa na Muumba wao kufika kutokana na ubovu ambao miili yao imetiwa na watesi wao!
Rais wangu, nawaombea afya njema wanawema hawa. Siku yao ya kuutoka ulimwengu huu wa mateso siijui kama ambavyo hata siku yangu mwenyewe pia siijui. Basi wacha niwalilie sasa na pia nijililie na mimi mwenyewe! Waliowatendea unyama huu mimi siwahukumu kwa sababu kuhukumu ni kazi yake Mungu. Watende lakini wajue kuwa hukumu ya Mwenyezi Mungu imesimama juu ya vichwa vyao.
Wajue pia kuwa hawataishi milele kusema watabaki kuilinda dunia, siku yao pia itafika nao watasimama mbele yake yeye aliye Muumba wao wote, wao watesi na wateswa wao. Siku hiyo, itakuwa ngumu kwao. Itakuwa siku ya kihoro. Mungu ni wa ajabu. Amewapangia kila mtu siku yake na atasimama mbele ya haki akiwa peke yake!
Nafsi zao zitawasuta na kuwajaza mateso ya uchungu mioyoni mwao yatokanayo na kuyakumbuka mateso waliowafanyia waja wa Mwenyezi Mungu. Nyongo itawakata maini watakapowaona wateswa wao wakiwa upande wa pili wa baba yao wakiimba na kumtukuza Mungu! Watatamani wawaombe msamaha kwa unyama waliowafanyia, lakini watakuwa wamechelewa!
Rais wangu, kwa sababu wahanga hawakuwanyang’anya mali yoyote waliokuwa nayo siku waliowafanyia unyama huo, basi lengo la uovu huu halikuwa ujambazi. Ndiyo kusema waliotenda unyama huu, hawakuwa majambazi. Sababu hii ndiyo inaitaka serikali iwajibike zaidi ili kujitoa katika tuhuma hizi zinazoelekezwa kwake.
Hata kama serikali itasema haikutenda unyama huu, kule kutowakamata wahusika kunawasukuma wananchi kuiona serikali yao kuwa mshirika katika kuwatesa na hata kuwaangamiza! Kwa ulinzi na upelelezi dhaifu kama huu, ni mwananchi gani atajiona yuko salama?
Ndugu rais, picha zilizowekwa gazetini zilikumbusha machungu mengi. Ilianza ya Absalom Kibanda. Alikuwa hana jicho moja. Lingine liling’olewa kinyama! Namfahamu Absalom. Alihariri makala zetu pale Free Media. Alifuatiwa na Steven Ulimboka akiwa mahututi! Amevimba mwili mzima! Kwa mara ya kwanza nimemwona Ulimboka uso kwa uso mwezi uliopita.
Nina kawaida ninaporudi kijijini kwangu Mbagala huwa napitia kijiwe changu cha zamani pale Uwanja wa Taifa. Kumbe siku hiyo Yanga walikuwa wanacheza. Sikuona mahali pa kuegesha mkweche wangu. Nikajikuta naitwa Mwalimu Mkuu njoo uweke hapa. Palikuwa na magari mengine. Nikamuuliza yule mtu, nikiegesha hapo hao nitakaowaziba watatokaje? Akaniambia weka tu najua wewe huendi mpirani. Sijui alijuaje. Mara ya mwisho nilienda Uwanja wa Taifa kuangalia mpira mwaka 1976.
Kwa mbele yangu kulikuwa na mwingine naye akiegesha gari lake. Aliposhuka nikamfananisha kisha nikamuuliza kama ndiye Steven Ulimboka, akasema ndiye. Nikamwomba nimsalimilie akanikubalia halafu hao wakaenda zao.
Sheikh Soraga na Padri Mwang’amba miili yao ilikuwa imeharibiwa vibaya. Unyama uliojidhihirisha wazi. Hawa nimewafahamu kupitia vyombo vya habari baada ya kukumbwa na majanga.
Rais wangu, ulimwengu umeendelea kujiuliza wana hawa walikosa nini hata kuwafanya wastahili adhabu ya mateso makali hivi? Walimkosea nani mkatili kiasi hiki? Hadi leo haijajulikana! Na kama aliyekosewa ndiye aliyetoa adhabu hizi, pia, hadi leo haijajulikana! Serikali imesema haihusiki. Aliyesema serikali inahusika ni nani? Huku ni kuyugayuga au kupaparika kunakosababisha kubabaika na hivyo kuifanya serikali ionekane inaweweseka.
Wa kuchonga hawakosekani hata msibani! Siku iliyofuata akatokea wa kutokea akasema kichwa kile cha habari kimeihusisha serikali na unyama ule. Akaahidi kuwa gazeti hilo litashughulikiwa kwa maana ya kulishikisha adabu! Haikujulikana mara moja kama mtu yule alikuwa anasema kwa kutumwa na serikali au alikuwa anajisemea mwenyewe. Kama alitumwa na serikali kwa hakika hiyo ni bahati mbaya. Anawafanya wanaosema serikali inaweweseka waonekane wanasema kweli. Kama alikuwa anatoa tu yake ya moyoni, basi ashindwe na alegee!
Rais wangu, wanasema kila mamlaka hutoka kwa Mungu. Ina maana kwamba Mwenyezi Mungu ameikabidhi serikali yetu wajibu wa kutunza na kulinda usalama na uhai wa watu wake walioko ndani ya nchi hii. Yanapotokea maafa kama haya yaliyowapata waja wake, Mwenyezi Mungu lazima amkamate au amuulize yule aliyemkabidhi dhamana ambaye ni serikali. Kama Mungu mwenyewe ataituhumu serikali kwa hili, wewe ni nani utake kuitoa serikali katika tuhuma hizi?
Sehemu zote tumeona, unapotokea uhalifu au wizi wa fedha au mali kwenye makampuni, viwanda au kwenye mashirika wa kwanza kukamatwa ni yule aliyekabidhiwa dhamana ya kutunza fedha au mali hiyo. Atashikiliwa hadi wahalifu wapatikane. Katika hali kama hii jitihada zozote zinazofanywa ili kuiondoa serikali katika tuhuma hizi ni sawa na kuweweseka. Mwenye jukumu na nyenzo zote za kuwakamata wahalifu wa unyama huu ni serikali yenyewe. Itaendelea kutuhumiwa hadi itakapowakamata watuhumiwa. Inaposhindwa kuwakamata watuhumiwa wakati kila siku inawakamata watuhumiwa wa maovu mengine wananchi wamtuhumu nani? Lazima wataendelea kuituhumu serikali. Kudhani kuwa leo hii bado wananchi wanaweza kuendelea kubabaishwa na mawazo mafupi ni kuweweseka pia! Kwa sababu ni kazi ya serikali kuwakamata wahalifu wa unyama huu, serikali haiwezi kukwepa kutuhumiwa. Siyo sawa hata kidogo kuwatisha wanaoituhumu serikali. Itaendelea kutuhumiwa kwa matukio haya hadi hapo itakapowakamata wahalifu. Kumbe atuhumiwe nani!

Jumanne, 24 Septemba 2013

MAGAIDI WAFELI JARIBIO LA KULIPUA BOMU HUKO DARAJANI VISIWANI ZANZIBAR USIKU WA KUAMKIA JANA...!

Watu wasiofahamika bado, usiku wa kuamkia jana Jumatatu walitupa kitu kinachosadikiwa kuwa bomu lililokuwa katika mfano wa 'sausage' karibu na eneo la biashara kando ya Barabara ya Darajani mjini Zanzibar.

UPDATES: JESHI LA KENYA LAFANIKIWA KUWAUA MAGAIDI 3 NA KUWANUSURU ZAIDI YA RAIA 200 KATIKA JENGO LA WESTAGE HIVI PUNDE...!!


NAIROBI; KENYA: Kenya Defence Forces ( KDF ) ina taarifa kwamba magaidi watatu wameuawa na Askari 11 wa kenya kujeruhiwa katika  operesheni ambayo imedumu kwa zaidi ya masaa 48.